Na Mwandishi Wetu
* Litafanyika Uwanja wa Taifa, aahidi makubwa
MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili
mwenye sauti nyororo, Upendo Kilahiro amekuwa wa kwanza kuthibitisha
kushiriki katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka
Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
tamasha hilo, Alex Msama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Msama Promotions, alisema Dar es Salaam kuwa Kilahiro amemthibitishia
kwamba atashiriki tamasha hilo.
"Kilahiro tutakuwa naye kwenye
tamasha, na naamini kwamba mwaka huu tamasha hili litakuwa bora zaidi
kutokana na kushirikisha waimbaji wengi wakali," alisema Msama.
Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo la
aina yake, baada ya kufanyika Dar es Salaam, pia litarindima kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9.
Tamasha la mwaka huu malengo yake
makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na
kuwasaidia mitaji wanawake wajane.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu
litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi kadhaa za
Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.
Akizungumza Dar es Salaam, Kilahiro
alisema amepania kufanya mambo makubwa katika tamasha la mwaka huu, na
atapanda jukwaani kuimba 'live' na bendi yake ya Upendo Kilahiro.
"Natoa mwito kwa mashabiki wangu
wasiwe na wasiwasi, watarajie kupata vitu vizuri na tofauti zaidi...
watapata vitu vinono kwa vile tamasha hili linazidi kuwa bora zaidi.
"Sikukuu ya Pasaka ni upatanisho
kutokana na kifo cha Yesu Kristo aliyefia msalabani na kufufuka siku ya
tatu... tutaienzi sikukuu hiyo kwa nderemo," alisema Upendo.
Mwanamuziki huyo anayeabudu katika
Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam (Kwa Askofu
Gamanywa), alisema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na
mbali na kufanya mazoezi, pia atafunga na kusali ili Mungu amfanyie
miujiza.
Aliwaomba mashabiki wamiminike kwa
wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 na Jamhuri Aprili 9,
kuona mambo mazuri aliyowaandalia na kuongeza kuwa kwa vile anamtukuza
Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini
atawapa kile wanachotaka kutoka kwakwe.
Alisema anatarajia kuimba nyimbo
mbalimbali zikiwemo zilizotamba za Zindonga (alioimba kwa Kizulu),
Unajibu Maombi na Ni Salama Rohoni. Kilahiro hivi sasa anatamba na
albamu yake mpya ya Ficho Langu aliyoirekodi nchini Canada.
Wednesday, February 22, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



0 Maoni::
Post a Comment