Kutokana na hali hiyo Zamalek walisema kama serikali itashikiria uamuzi wa kuzuia mechi za soka kuchezwa nchini Misri watalazimika kucheza mechi yao ya marudiano na Yanga nje katika nchi ya Algeria au Sudan.
“Tunatumaini tutafahamu vizuri kuhusu hali ya usalama hapa na kama serikali itatupa ruhusu ya kucheza mchezo wetu hapa au laa,” alisema msemaji wa Zamalek, Ali Aboul-Naga Said.
Zamalek imepokea maombi kutoka klabu ya Algeria, ES Setif na Hilal ya Sudan kuwa wenyeji wa miamba hiyo ya Cairo inayopewa nafasi ya kusonga mbele baada ya kupata sare ya 1-1 ugenini Jumamosi iliyopita.
Lakini, jana serikali ya kijeshi ya Misri ilitoa ruksa kwa Zamalek kucheza mechi hiyo nyumbani kwenye uwanja wa chuo cha jeshi uliojengwa mwaka 1989 kwa lengo la kutumika kwa michezo ya majeshi pekee ukiwa kwenye Mtaa wa Onouba kaskazini mwa jiji la Cairo umbali wa maili 7 kutoka uwanja wa kimataifa wa Cairo.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema wapo tayari kukabiliana na Zamalek katika nchi yoyote kwenye mchezo wao wa marudio.
Mechi hiyo itachezwa bila ya mashabiki kutokana na Shirikisho la Soka Afrika, CAF kuwafungia mashabiki wa Zamalek kutokana na vurugu walizofanya kwenye mchezo dhidi ya Club Africain ya Tunisia uliofanyika mwaka jana kwenye uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Zamalek ilitwaa ubingwa mara ya mwisho wa Afrika mwaka 2002, wiki iliyopita ili nusurika kipigo baada ya kupata sare ya 1-1 na Yanga kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Zamalek wanategemea kurejea kwa wachezaji wake majeruhi katika mchezo huo kutawafaidia watapocheza dhidi ya Yanga hapo Cairo.


0 Maoni::
Post a Comment